Jumuiya ya Wanafunzi na Vijana wa Kiislam Tanzania (TAMSYA) Mkoa wa Katavi
imehitimusha maadhimisho ya Hijab Day 2026 kwa kutoa elimu na kuhamasisha uvaaji wa hijab ya kisheria kwa wanafunzi na wanawake kwa kuzingatia maadili na mafundisho ya Kiislamu. Maadhimisho hayo yalijumuisha utoaji wa mada mbalimbali zilizolenga kuonesha nafasi ya hijab katika kujenga heshima, utambulisho na maadili katika jamii.
Mgeni rasmi alikuwa Mheshimiwa Bi. Roza Nabahan, Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Tanganyika, ambaye alishiriki pamoja na kutoa ujumbe wa kuhimiza jamii kuendelea kuthamini elimu na maadili.
Kilele cha maadhimisho kilifanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Mpanda, ambapo jumla ya hijab 123 ziligawiwa kwa washiriki ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha uvaaji wa hijab ya kisheria. Aidha,
kulikuwa na mfano wa uvaaji wa hijab kwa mwanamke mmoja ili kuonesha namna inayopaswa kuvaliwa na wanawake katika maisha ya kila siku, wakiwa majumbani na katika maeneo ya wazi kwa kuzingatia staha na maadili ya Kiislamu.
Sambamba na maadhimisho hayo, kulifanyika pia zoezi la uchangiaji damu salama, ambapo jumla ya chupa 23 za damu zilipatikana kupitia washiriki waliojitokeza kuchangia.
*Imeandaliwa na Idara ya Habari, Uhusiano na Ustawi wa Jamii – TAMSYA Mkoa wa Katavi.*